top of page

Safari ya Lenaida hadi kuanzisha kituo cha kulea watoto

Updated: Mar 26

Vijana walio wengi wakiingia kwenye ajira hudumaa kifikra na kusahau malengo yao hivyo waweke mbele dhamira zao na kuzipigania.


Na Anord Kailembo


Naitwa Lenaida Sylvester mmiliki wa kituo cha kulea watoto cha Tegemeo Montessori kilichoko mtaa wa Mafumbo kata Kashai manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.



Wakati nikiwa mdogo nilikuwa nikipenda kushona nguo, nilipokuwa nikiona mabinti wakishona nguo na mimi nilitamani niwe kama wao maana karibu na nyumbani kulikuwa na kituo cha kushona nguo ambapo mafundi walikutana na kufanya shughuli zao za ushonaji  na wakati huo nilikuwa nasoma shule ya msingi.


Nilipomaliza darasa la 7 nikajiunga na kituo cha maarifa ya nyumbani (Homecraft) hapo nilichukua masomo ya upishi, ufumaji, ushonaji na malezi ya watoto wadogo.


Nilikaa pale kwa miaka miwili na baada ya kuhitimu nikaajiriwa na shirika la Partage Tanzania kama mpishi wa chakula cha watoto waliokuwa wakisomeshwa na shirika hilo kwenye kituo cha Montessori Kabyaile kilichoko kata Ishozi wilayani Missenyi kwa kipindi cha miaka minne.


Wakati nikiwa  hapo nilitokea kupenda sana malezi ya watoto wadogo na hii ilichagizwa zaidi na mafunzo ya malezi niliyokuwa nimeyapata chuoni, hivyo mbali na mapishi nikawa naingia darasani kufundisha watoto kama msaidizi.


Kadri nilivyokuwa karibu na watoto kwa kuwapikia na kuwahudumia sambamba na kuwafundisha, ikanifanya zaidi kuisahau ndoto yangu ya tangu utoto ya kuwa fundi cheleani na badala yake kuwaza kuwahudumia watoto katika nyanja ya malezi na elimu.


Baadhi ya watoto wa Tegemeo Montessori wakicheza

Wakati nikiendelea kutekeleza wajibu wangu huo mwajiri wangu akavutiwa na namna ninavyoshiriki kujitolea na kuniwezesha kwenda chuo cha Partage Montessori kusomea malezi ya watoto; Nilijisikia furaha sana kwa sababu ni kama niliona matamanio yangu niliyokuwa nayo moyoni ya kuwahudumia watoto yakifanikiwa.


Mbali na furaha niliyokuwa nayo, pia niliumia kuona naiacha jamii ya watoto iliyokuwa inanipenda sana na tulikuwa tayari tumezoeana kiasi cha kutosha lakini ilinibidi niwaache ili niende kuongeza maarifa zaidi ya kuwahudumia.


Nilisoma miaka 2 kuanza mwaka 2007 hadi 2009, licha ya kuwa na elimu ya malezi sambamba na kufundisha kabla ya kwenda chuoni lakini nilikutana na elimu na maarifa mapya yaliyonijenga na kunifanya kumpenda mtoto zaidi sambamba na kuipambania ndoto yangu mpya ya kuwa mwalimu.


Masomo yaliambatana na mafunzo ya vitendo hivyo yalinijenga katika namna ya kutenda zaidi na pia nakumbuka baada ya kuhitimu masomo yangu niliajiriwa na Partage kuwa mwalimu mlezi katika kituo cha Kikukwe.


Nilihudumu katika ajira hiyo kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 baada ya hapo kituo kilifungwa, lakini namshukuru aliyekuwa mwajiri wangu kwani aliniachia vifaa vyote vya ufundishaji hivyo ikanitia moyo wa kuendeleza huduma kwa jamii iliyozunguka eneo lile.


Baada ya kuachiwa kituo baadhi ya wazazi walishindwa kumudu kulipa karo hivyo kufanya uendeshaji wa kituo kusuasua, hali hiyo ilinifanya nihamie mjini Bukoba kuanzisha kituo changu binafsi.


Haikuwa rahisi maana changamoto zilikuwa ni nyingi, ilikuwa ni safari iliyokuwa na giza mbele nikijiuliza naenda kuanzia wapi? Nikakumbua wakati nasoma chuo katika pitapita zangu mtaani jirani na nilipokuwa nikipanga, kulikuwa na kijana mmoja fundi selemara aliyekuwa akitutengenezea zana za ufundishaji.


Katika eneo alilokuwa akifanyia shughuli zake kulikuwa na nyumba zisizokuwa na wapangaji akili yangu ikanielekeza kumfuata kijana huyo ili anisaidie kupata nyumba hizo kwa ajili ya kuanzisha kituo.


Baadhi ya watoto wa Tegemeo Montessori wakijifunza kwa mifumo tofauti


Mungu si Athumani nyumba zile nikakuta bado hazikaliwi na mtu na yule kijana akanielekeza kwa mwenye nazo, nilipokutana na mwenye nyumba na kumueleza lengo langu hakusita akanikubalia na mchakato huo ulichukua miezi 2.


Nakumbuka ilikuwa mwezi wa desemba wakati wa likizo, hivyo baada ya kupata eneo la kufundishia, vyumba viwili vya madarasa nikaanza kupita nyumba kwa nyumba nikiomba wazazi wanipatie watoto wa kufundisha lengo likiwa kufikia mwezi januari zinapofunguliwa shule basi niwe tayari na wanafunzi wa kuanzia.


Ilikuwa ni ngumu kuaminika kwa wazazi na hadi naifikia januari nilikuwa na watoto 3! tu, na wazazi wengi walikosa imani kwa sababu ya kituo kuanza maana walio wengi wanaamini sana vituo ambavyo tayari vimeanza kwani wanajua ufundishaji wao na mazingira kwa ujumla.


Sikujali ni watoto wangapi nilikuwa nao na wakati huo, niliamini siku moja nitaifikia ndoto yangu ya kuwa na wanafunzi wa kutosha na kufikia mwezi desemba mwaka 2014 nilikuwa na wanafunzi 12.


Kutokuwa na utoshelevu wa wanafunzi kulinifanya gharama nyingi za uendeshaji na kodi kuzibeba mwenyewe kupitia vyanzo vingine vya fedha.


Watoto hao 12 walionesha maajabu makubwa kutokana na elimu ya Montessori waliyokuwa wakifundishwa shuleni, mbali na kujua kusoma, kuandika na kujieleza pia waliweza kufanya kwa vitendo shughuli mbalimbali za nyumbani ikiwemo kufua, kuosha vyombo, kufanya usafi n.k.


Hii ilifanya mwaka uliofuata kupata wanafunzi wengi zaidi ya mwaka 2014 ambapo januari nilipokea wanafunzi 36! kusema kweli nilipiga magoti na kumshukuru Mungu maana nilikuwa na maswali mengi kichwani, ikiwemo kumudu kuendesha kituo.


Nilishangaa sana kadri muda ulivyozidi kusogea wanafunzi waliongezeka zaidi hadi mwishoni mwa mwaka nilikuwa na watoto 76, nikaanza kuwaza ni wapi nitahamia maana madarasa yote yalijaa wanafunzi.


Nakumbuka nilimfuata mwenye nyumba kumuomba kufanya upanuzi wa jengo lake, kuongeza madarasa zaidi lakini pia kuongeza idadi ya vyoo na kwa bahati mbaya hakunikubalia hivyo nikaingiwa na wazo la kununua kiwanja ili nijenge.


Kipindi hicho natafuta fedha kwa ajili ya kiwanja ilibidi niweke ukomo wa idadi ya watoto kupokelewa kituoni hapo ambayo ilikuwa ni watoto 80, chakushangaza wazazi walikuwa wakizigombania yaani wanawaandikisha watoto mapema sana kabla ya uandikishaji.


Mwaka 2017 nikanunua kiwanja na kuanza kujenga na hadi kukamilika ilikuwa mwaka 2021 ndipo rasmi nikahamia kwenye kituo changu kilichonipa uhuru wa kuchukua idadi zaidi ya watoto kwani katika upande wa miundombinu nilianza na madarasa 2.


Mwanzoni niliogopa hasa kuhusu ujenzi nikijiuliza nitaweza? Lakini mwalimu wangu wa chuo na rafiki yangu karibu madame Jacqueline Mwombeki alinitia moyo na kuniwezesha kupata ramani kwa gharama zake, na hadi ujenzi unakamilika nilikuwa naye bega kwa bega.


Licha ya kutokufurahia kitendo cha mwenye nyumba kuzuia upanuzi wa nyumba yake kwa ajili ya madarasa, lakini namshukuru sana kwa sababu maamuzi yake ndiyo yaliyozalisha wazo jipya la kununua kiwanja na kujenga kituo changu.


Baada ya kuanza huduma kwenye kituo changu ziliibuka changamoto ukizingatia kuwa nimebadilisha mazingira ya kazi hivyo ilinihitaji zaidi kuwashawishi wazazi wa maeno nilikohamia sambamba na kule nilikokuwa awali waweze kunipatia watoto wao.


Kwa sasa ninayo miaka 4 tangu nimehamia kwenye kituo changu na mshukuru sana Mwenyezi Mungu maana jamii imeendelea kuniamini lakini pia ameniwezesha, nimemudu kuandaa mazingira ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya elimu.


Ninayo jumla ya madarasa mawili, ofisi na chumba cha mwalimu, kutoka kuajiri walimu wawili hadi kufikia walimu, mpishi mmoja na sote tunawahudumia watoto 44 tulionao kwa sasa.


Inaweza ikwa inachekesha lakini ndivyo ilivyo, wakati wamiliki wengi wa vituo kama cha kwangu wakitamani kumiliki shule kubwa zaidi ya kituo, mimi binafsi natamani niwe na kituo kikubwa cha kuhudumia watoto wadogo pekee, hii ni kwa sababu tangu mwanzo napata elimu ya malezi nilitokea sana kupenda watoto wadogo.


Changamoto

Ninalo eneo la kutosha kujenga miundombinu mingi zaidi ya watoto lakini kutokana na changamoto ya kifedha nimeshindwa kuweka miundombinu hiyo, mfano kuongeza madarasa, vifaa vya michezo na nyumba za walimu, hivyo iwapo kuna mfadhili aweze kunisaidia.

Ushauri

Kwanza ushauri wangu kwa vijana wanaosoma na wenye ndoto ya kumiliki kituo au shule, wanatakiwa watoe fikra za kuajiriwa vichwani mwao, wajiande mapema kisaikolojia kuwa wanaenda kuweka ndoto zao katika vitendo baada ya kuhitimu.


Vijana walio wengi wakiingia kwenye ajira hudumaa kifikra na kusahau malengo yao hivyo waweke mbele dhamira zao na kuzipigania.


Pili, nawashukuru wazazi wanaoamini kituo changu na pia nawashauri wengine waendelee kuwaleta watoto wao kwani kituo changu kinasimamia misingi ya malezi kwa watoto, usalama pamoja na kuiishi misingi na miongozo ya malezi na makuzi ya watoto.


Kituo changu kinaitwa Tegemeo Montessori kinachopatikana mtaa Mafumbo kata Kashai manispaa ya Bukoba mkoani Kagera karibu kwa mawasiliano zaidi piga simu No. 0763817544.

Comments


bottom of page