Maelekeo yako usukani wa maisha yako (1)
- Jacqueline Mwombeki
- Mar 3
- 5 min read
Updated: Apr 17
Na Jacqueline Mwombeki
Maria Montessori anatukumbusha kuwa binadamu ni yule yule tangu dunia kuumbwa na mahitaji yake ya msingi hayajawahi kubadilika na hata namna ya kujidhihirisha ni ile ile. Lakini kwa vile binadamu amepewa uwezo wa kutaka kujua zaidi, huonekana ni muhitaji daima na kwa maana hiyo hakuna ngazi anayoifikia kimaisha inayoweza kumridhisha.
Kwa umuhimu wa takwa hilo hatuwezi kumbadilisha na wala hahitaji kubadilishwa kwani asili haikumwekea kikomo cha maarifa ila, kupitia kiu yake ya kutaka kujua hili na lile, anaweza kujifunza kuwa na mipaka. Na ili awe na mipaka ni lazima ajenge utambuzi na kujizuia kuvuka mipaka yoyote iliyo hatarishi na isiyo salama kwake na kwa wengine kwani kila mwanadamu ameumbiwa uwezo huo.
Katika ukuaji tunatambua kuwa tunapita hatua moja kwenda hatua nyingine lakini utu wa mtu kamwe, haujawahi kubadilika na hii ni kwa sababu mwanadamu anaweza kuwa na maendeleo kielimu na kiuchumi, ila maelekeo ndani ya mwanadamu ni yale yale tangu kuumbwa kwake.
Tukijiuliza kwa swali la kawaida; hivi ni nani hapendi kuteta?... Je, ni nani hasumbuliwi na mambo kutokuwa na utaratibu, lakini pia je, ni nani anaweza kukaa siku nzima pasipo kujitingisha ama kujongea kama yeye hana changamoto ya kiafya, na je ,ni nani anaweza kukaa dakika moja hajafikiri pamoja na kwamba hapa jibu lako laweza kuwa kwamba tunapokuwa tumesisinzia mara nyingi huwa hatufikiri.
Hayo ni baadhi ya maekeleo ya binadamu anayoyaishi maisha yake yote japo yanaweza kudhihirishwa na mwenye nayo kwa viwango tofauti kulingana na elimu na malezi anavyovipokea mtu husika kutoka kwenye mazingira yake kwani tabia huzaliwa ndani ya maelekeo.
Maelekeo
Kwa tafsiri ya Oxford Maelekeo ni hali ya kuelekea ama kuendea jambo fulani kwa kulikubali ama kulikataa. Ni asili inayopelekea kiumbe kutembea katika mfumo wake wa maisha ambayo huwezesha viumbe kazi ya kuzaliana, kukabiliana na mazingira na mfumo wa maisha kwa lengo la kuendelea kuishi.
Hizi ni sheria za asili zinazobainisha uwepo wa maisha ya aina fulani ambazo pasipo kuzivunja huishi ndani ya maisha husika na tunaweza kusema kuwa ndiyo namna ya kuishi kwani kiumbe kisichofanya hivyo, hakina maisha. Kila elekeo lina uzuri na ubaya wake na kama elekeo zuri haliko kazini, elekeo baya liko kazini.
Naweza kusema kuwa wema, fadhila na utambuzi, hupelekea maelekeo mazuri kujitokeza kwa wingi ambapo maslahi na kupuuza hupelekea maelekeo mabaya kujitokeza wakati wa jambo fulani.
Maneno ya Mungu yanatwambia kuwa amempa uwezo mwanadamu kutawala dunia na vyote vilivyomo. Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema kuwa dunia ndiyo maelekeo na vyote vilivyomo na kutawala ni ule uwezo wa kuchangua kuelekea kwani mpaka mtu aseme hili nalitawala, ni lazima liwe ndani ya uwezo wake na awe anatambua miliki zake.
Katika uchunguzi wake, Dr. Maria Montessori amebaini kuwa binadamu anayo maelekeo yanayomwongoza mtu kutenda jambo kwa kukusudia tofauti na ilivyo kwa viumbe wengine
ambao hufanya vitu kwa kuongozwa na silika zisizoweza kutawaliwa na kiumbe huyo.
Maelekeo hutawala mfumo mzima wa mawasiliano, hisia na tabia ambavyo hupelekea kiumbe fulani kuishi na kutenda sawa na maumbile yake tofauti na kiumbe wa aina nyingine.
Imechunguzwa na kuthibitishwa kuwa maisha ambayo viumbe wengine wanayaishi wangekuwa na maamuzi juu yake, wangetamani kuyaishi tofauti. Kwa bahati mbaya chaguo la kufanya hivyo yaani kutawala silika hawakupewa.
Labda swali linaweza kuwa kama sisi hatufungwi na sheria hiyo ya kutawaliwa na silika zetu, mbona wengi tunaishia kuwa kama fulani na pengine tusifikie viwango tunavyotarajia? Jibu langu laweza kuwa kwamba mtoto wa binadamu anapozaliwa anakuta tayari mazingira yameandaliwa kwa maana ya kwamba yupo wa kumpokea, yupo wa kumuhudumia, yupo wa kumuongoza na yupo wa kumlinda na hayo yasipofanyika kweli mtoto wa binadamu hawezi kuishi; tofauti na ilivyo kwa viumbe wengine.
Mimea kwa kutumia hisia hunajua ni wapi itaweka mizizi, ndama anajua afanyeje ili apate kunyonya, kinda la ndege pia wakati ukifika linajua lifanyeje ili litoke kwenye ganda na kuwa chakula kikiletwa lisipoachama mama kinda hana uwezo wa kuliachamisha, wadudu nao baada ya kuzaliwa tu, imekula kwao, nk; hali mtoto wa binadamu ni mzigo mzito ama ni msalaba kwa mbebaji. Je, tuuone kweli ni msalaba?
Kwa maisha ya siku hizi mzazi anaweza kuona ni msalaba. Ila kabla hujafikiria kwenda huko ebu turudi kwenye ukweli ambapo katika viumbe waliotajwa, ni binadamu tu anayezaliwa maskini wa hali zote, iwe ni kuongea, kujongea, kutambua, kufikiri, na hata pengine viumbe wengine wangekuwa wanazaliwa na dhana ya uchumi bado mtoto wa binadamu angeonekana kuchelewa kutambua elimu ya uchumi.
Mtoto wa binadamu utamvika kwa kuwa hana nguo, utamlisha kwa kuwa hana chakula na utamtunza kwa kuwa hana hifadhi, utamwongoza kwa kuwa hajui pa kuekelea. Na hii yote humfanya mzazi ahisi uchovu.
Ukijua ni kwa nini mtoto wa binadamu anazaliwa hivyo, ni lazima upatwe na huruma kwani hakuchagua kuzaliwa hivyo. Lakini pia huyu ni yule binadamu unayemtaka kesho awe mrithi wa mali zako, kizazi chako na wa Taifa lako, na hata pia adumishe afya, nk. Maandalizi ya kumfanya kuwa vile yaani mrithi hayana ughafla na hayakwepeki, uwe navyo na usiwe navyo.
Binadamu hawezi kufananishwa na myama, tumepambanuliwa kama ambavyo kila kiumbe kina upekee wake. Ndivyo ilivyo na katika matumizi ya maelekeo mnyama anazaliwa anajua kuthubutu na ndio maana kwa bidii na hiari anaishi.
Wanyama na viumbe wengine wakiwa wanatawaliwa na silika za kurithi, binadamu anaongozwa na silika anazoweza kutawala ambazo hayo ndiyo maelekeo yanayomsukuma kufanya au kutofanya, kupenda na kutopenda, kujali ama kupuuza, kulaani au kubariki, kulalamika au kushukuru, kuthamini au kuharibu, kuthubutu au kujaribu, hofu au ujasiri, woga, wizi, uvivu na mengine mengi yafananayo na hayo na roho zote za uharibifu.
Maelekeo ni usukani wako
Uwe umepanda baiskeli, pikipiki au chombo chochote cha moto, usukani wa chombo hicho ni sawa na maelekeo yako kwa kuwa unaweza kuamua kufanya vyovyote kwa muda huo.
Maamuzi wakati wote huwa ni magumu na wala haitofautiani na maamuzi unayoyafanya unapokuwa kwenye usukani na hivyo ndivyo unavyoweza kuamua kufanya na maelekeo yako yanapojitokeza kwani mwenye nguvu na utashi wa kuyatawala au kuyaacha yakutawale kama ilivyo kwa viumbe wengine ni wewe.
Kupitia Montessori tunatambua kwamba, ni mambo mengi ambayo tunaweza kuyafanyia kazi kwenye umri mdogo wa mtoto ambayo tusipofanya hivyo tunakuja kuona matokeo yake kwamba baadaye vijana hushindwa kuhimiri vishindo kutokana na ukosefu wa misingi thabiti katika ukuaji wao ambayo humpelekea mtoto kutojisamehe na hivyo kuishi na makovu hayo mpaka uzeeni.
Montessori anatukumbusha kuwa mtoto wa mwanadamu hakui kama ukuavyo mmea au kitu kingine na pengine tunaweza kufikiri kwamba baada ya kuzaa kazi inakuwa imerahisishwa kweli kweli katika hatua hiyo na nyingine zinazofuata na yeyote anayemtakia mema mtoto au kijana atamjali, atamlinda, atamtunza na kumuongoza, atamheshimu, atamuombea mema, na hatamuacha aanguke.
Wengine tunafikiri kuwa hakuna kazi iliyo ngumu kama kumleta mtoto duniani lakini nataka nikwambie kuwa hakuna fainali iliyo ngumu kama malezi unayompa mwanao. Ujenzi wa binadamu huanza tu baada ya mtoto kuzaliwa na hata katika hatua zinazofuata, tunachokijua kwa wingi ni kumtunza kwa kujaribisha kupitia hatua za kutunza mmea tukiwa tunadhani kuwa tunaweza kumlea mtoto kama tunavyoona mmea ukikua hadi amekuwa.
Kwa wepesi huo na unafuu tunaouona, tunapangusa mikono na kusubiri kitakachotokea huku tukiwa bado tunatamani mtoto asihoji chochote yaani tunataka afanane kabisa na viumbe wengine wasiozungumza tukiwa tunasahau kwamba huyu ni binadamu anayeongea, aliye na mahitaji lakini pia mwenye maamuzi.
Ili elimu iwe msaada wa maisha ya mwanadamu ni lazima kuhudumia upekee wa mtoto, kwa kuhusisha elimu hiyo na saikolojia jambo litakalowezesha kumjua vizuri tunaye muhudumia. Kupitia mbinu na falsafa zinazotolewa kwenye makala hizi, kutakuwa na mwendelezo wa maudhui yanayolenga mtu kujitambua zaidi, kujikubali na kuchukua hatua katika nyanja za kielimu, kujitegemea, kuwajibika na kubaki katika misingi bora ya utu.
Ili kutengeneza vizazi/kizazi chenye afya ya mwili na akili ni lazima tutambue kwanza umuhimu wa maelekeo ya binadamu kwa kuendelea kufuatilia makala za mbinu na falsafa za Montessori zinazolenga kuelimisha juu ya elimu, malezi, makuzi na kukuza fikra tunduizi chanya, katika hali ya kukabiliana na masuala mtambuka, vijana kujitambua, kujithamini na kuwajibika vitakavyoendeleza utamaduni wa wetu na kuendelea kuzalisha raia wema na bora.
Tafadhali fuatilia mwendelezo wa makala hii katika toleo lijalo…
Comments