HEKMA, SILAHA YA KIMYA
- 21 hours ago
- 4 min read
Katika dunia ya leo yenye haraka nyingi, hasira za ghafla, ushindani usio na mwisho na maamuzi ya papara, kuna jambo moja ambalo linaendelea kupotea taratibu lakini lina thamani kubwa kuliko mali, elimu au hata nguvu, jambo hilo ni hekima.
Watu wengi wana elimu lakini hawana hekima ya kutumia elimu hiyo. Wengine wana fedha nyingi lakini hawana busara ya kuzitumia. Kuna wenye madaraka makubwa lakini wanashindwa kuyaongoza maisha yao binafsi, hii inaonyesha wazi kuwa mafanikio ya kweli hayategemei tu akili au uwezo wa kufanya kazi, bali yanahitaji hekima.
Hekima ni uwezo wa kutumia maarifa, uzoefu na akili kwa njia sahihi ili kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yako na ya wengine, hekima humfanya mtu ajue wakati wa kuzungumza na wakati wa kunyamaza, wakati wa kupambana na wakati wa kuondoka kimya kimya.
Leo hii migogoro mingi ya kifamilia, urafiki unaovunjika, ndoa zinazoparaganyika na hata vita vya maneno mitandaoni havitokani na ukosefu wa elimu bali ukosefu wa hekima, tunapo angalia jamii ya sasa tunaona watu wengi wanakimbilia kujibu kabla ya kuelewa, mtu anakasirika kwa sekunde chache na kuharibu uhusiano wa miaka mingi, wengine wanaamua kuandika maneno makali mitandaoni bila kufikiri madhara yake.
Kuna wanaopoteza kazi kwa sababu ya ulimi wao, wengine wanapoteza ndoa kwa sababu ya kiburi, na wengine wanapoteza marafiki kwa sababu ya kushindwa kutumia hekima katika maneno yao.
Mara nyingi mtu mwenye hekima haonekani kuwa mshindi wa haraka, lakini mwisho wa siku ndiye anayebaki salama, hekima humzuia mtu kufanya maamuzi ya muda mfupi yatakayomgharimu maisha yote, kuna watu leo wanajuta kwa sentensi moja waliyoizungumza kwa hasira.
Kuna wazazi wanalia kwa sababu hawakutumia hekima katika malezi ya watoto wao. Kuna viongozi waliopoteza heshima kwa sababu ya maamuzi ya haraka yasiyo na busara. Hekima ni kama breki ya gari. Unaweza kuwa na injini yenye nguvu, lakini bila breki utasababisha ajali.
Mtu mwenye hekima si lazima awe tajiri au maarufu. Mara nyingi watu wenye hekima huonekana watulivu na wenye uvumilivu mkubwa, hawapendi kubishana kila mahali na hawalazimishi kushinda kila mjadala.
Wanajua kuwa si kila vita vinahitaji kupiganwa, wakati mwingine hekima ni kunyamaza wakati una uwezo wa kujibu, wakati mwingine hekima ni kuondoka mahali ambapo heshima yako haithaminiwi na wakati mwingine hekima ni kukubali kosa hata kama linauma.
Katika maisha ya kawaida tunakutana na watu wanaojiona wajanja kwa sababu wanaweza kujibu kila kitu, kubeza wengine au kuwashusha wenzao mbele za watu lakini ukweli ni kwamba busara ya kweli haimfanyi mtu awe na kiburi.
Hekima huambatana na unyenyekevu, kadri mtu anavyokuwa na hekima ndivyo anavyozidi kuelewa kuwa maisha si mashindano ya nani anasema sana, bali nani anaishi vizuri na wengine.
Familia nyingi leo zimepoteza amani kwa sababu ya kukosekana kwa hekima. Kuna watoto hawazungumzi na wazazi wao, ndugu hawasalimiani kwa miaka mingi na wanandoa wanaishi nyumba moja lakini mioyo yao ipo mbali, sababu kubwa si umaskini pekee, bali ukosefu wa hekima.
Mume mwenye hekima hawezi kutumia hasira kuongoza familia yake, mke mwenye hekima hawezi kutumia maneno ya kejeli kujenga ndoa yake, mzazi mwenye hekima hujua kuwa mtoto hafundishwi kwa kipigo pekee bali kwa mfano wa maisha.
Wakati mwingine familia haihitaji pesa nyingi ili iwe na amani, inahitaji watu wachache wenye hekima ya kusamehe, kusikiliza na kuvumiliana, kuna nyumba zimejaa vitu vizuri lakini hakuna furaha, na kuna nyumba maskini lakini zimejaa upendo na amani kwa sababu ya hekima.
Katika zama hizi za teknolojia na mitandao ya kijamii, watu wengi wanataka kuonekana kuliko kueleweka, watu wanapima thamani ya maisha kwa likes, followers na comments.
Wengine wamegeuza matusi kuwa ujasiri na kejeli kuwa umaarufu, lakini mtu mwenye hekima hujua kuwa si kila jambo lazima lichapishwe, kuna maumivu yanahitaji sala, si status, kuna migogoro inahitaji mazungumzo, si live stream.
Wapo waliopoteza kazi kwa post moja, waliopoteza ndoa kwa ujumbe mmoja na waliopoteza heshima kwa dakika chache za hasira mtandaoni, hekima hutufundisha kufikiri kabla ya kutenda, kabla ya kutuma ujumbe, ni muhimu kujiuliza kama maneno hayo yatajenga au kubomoa, kama yakisomwa kesho yataendelea kuleta heshima au majuto, maswali hayo madogo yanaweza kuokoa maisha, kazi na mahusiano mengi.
Fedha zinaweza kuibwa, umaarufu unaweza kupotea na uzuri wa sura unaweza kuzeeka, lakini hekima ni utajiri ambao mtu akipata huwa sehemu ya maisha yake, mtu mwenye hekima hata akiwa maskini bado ataheshimiwa, lakini mtu asiye na hekima hata akiwa tajiri ataishi kwenye migogoro.
Hekima humsaidia mtu kujua marafiki wa kweli, kutumia fedha vizuri, kuishi kwa nidhamu na kufanya maamuzi sahihi, watu wengi wameingia kwenye madeni, mahusiano mabaya au biashara za hasara kwa sababu walitanguliza tamaa badala ya hekima.
Ndiyo maana wazee wengi wenye uzoefu mkubwa huwa na maneno machache lakini yenye uzito mkubwa, maisha huwafundisha kuwa si kila jambo linahitaji hasira, si kila changamoto inahitaji vita na si kila tofauti ya mawazo inahitaji uadui.
Katika maisha ya kiroho, hekima ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Mwanadamu anaweza kuwa na kila kitu lakini bila hekima akaanguka, historia inaonyesha kuwa watu wengi waliopata mamlaka, utajiri na umaarufu walianguka kwa sababu walikosa hekima ya kuvitumia walivyopewa.
Hekima ndiyo humfanya mtu awe na kiasi, awe na huruma na awe na uwezo wa kuona mbali kabla ya kufanya maamuzi, ndiyo maana kila siku mwanadamu anapaswa kujiuliza kama anaishi kwa hasira au kwa hekima, kama anaamua kwa papara au kwa busara, kama anajenga watu au anawabomoa.
Mwisho wa maisha, watu hawatakumbuka ulivaa nguo gani, ulikuwa na simu ya aina gani au uliendesha gari la thamani gani, watakumbuka ulivyowatendea. Watakumbuka maneno yako na namna ulivyowafanya wajisikie, mtu mwenye hekima huacha alama nzuri hata baada ya kuondoka duniani.
Huacha familia yenye umoja, huacha marafiki wenye kumbukumbu njema na huacha jamii iliyojifunza kitu kupitia maisha yake, lakini mtu asiye na hekima huacha majeraha, chuki na majuto.
Katika dunia ambayo kila mtu anataka kusikika, kuwa mtu mwenye hekima ni zawadi adimu. Hekima si udhaifu wala si woga, hekima ni nguvu ya ndani inayomfanya mwanadamu ashinde bila kuharibu wengine, kama una elimu, ongeza hekima. Kama una fedha, tumia hekima.
Kama una mamlaka, ongoza kwa hekima na kama una maumivu moyoni, yashughulikie kwa hekima, kwa sababu mwisho wa siku maisha mazuri hayajengwi na nguvu pekee, bali yanajengwa na maamuzi sahihi, na maamuzi sahihi huzaliwa na hekima.




Comments