top of page

Bidii

  • 6 days ago
  • 3 min read

Simama tena, Anza tena, Pambana tena

Kuna nyakati maisha humfanya mwanadamu ajione amechelewa. Ndoto zinapovunjika, mipango inaposhindikana, na milango mingi inapofungwa mbele yake, moyo huanza kukata tamaa polepole, wengine huacha kabisa kuamini kama wanaweza tena kufanikiwa.


Lakini historia ya maisha imeendelea kuthibitisha jambo moja kubwa kuwa si kila aliyeanguka ameshindwa, na si kila aliyechelewa amepoteza maisha, mara nyingi kinachomrudisha mtu kwenye mstari wa ushindi si bahati, si urithi, wala miujiza ya ghafla… bali ni BIDII.

 

Bidii ni silaha ya watu walioamua kutokukubali kushindwa, ni ule uwezo wa kuamka asubuhi hata wakati moyo umechoka, ni ile nguvu ya kuendelea kupambana hata pale ambapo hakuna anayekuamini tena.

 

Watu wengi duniani wamewahi kupita katika kipindi kigumu; wengine walikosa kazi, wengine walifeli masomo, wengine walidharauliwa, na wengine waliwahi kuambiwa hawataweza kufika popote, lakini walichagua kufanya jambo moja muhimu sana hawakusimama.

 

Mara nyingi jamii huona matokeo lakini haisemi kuhusu machozi yaliyotangulia mafanikio hayo. Tunawaona watu wakimiliki biashara kubwa, wakiongoza taasisi, wakijenga familia nzuri, au wakitimiza ndoto zao, lakini hatuoni usiku waliokesha wakihangaika, kukataliwa walikokupitia, wala mapambano waliyoishi kimya kimya, ukweli ni kwamba hakuna mafanikio ya kweli yasiyo na bidii nyuma yake.

 

Kuna vijana wengi leo wamekata tamaa kwa sababu maisha yao hayaendi kwa kasi waliyoitarajia, wanaangalia wenzao wakifanikiwa mitandaoni, wakinunua magari, wakijenga nyumba, na wao wanajiuliza kwanini maisha yao bado yako palepale.

Jambo moja muhimu wanapaswa kulielewa ni kwamba kila mtu ana safari yake. Mbegu hazichanui kwa siku moja, kuna ndoto zinahitaji uvumilivu, maombi, machozi na bidii ya muda mrefu kabla hazijatoa matunda.

 

Hakuna jambo lenye nguvu kama mtu aliyeamua kuanza tena, maisha yanaweza kukuangusha leo, lakini bado una nafasi ya kusimama kesho.

Unaweza kuwa ulifeli biashara, ukakataliwa kazi, ukaachwa, ukadharauliwa, au ukapoteza kila kitu ulichoamini kingekusaidia maishani, lakini bado mwisho wa maisha yako haujaandikwa, kadiri moyo wako unavyoendelea kupigana, bado kuna nafasi ya ushindi mbele yako.

 

Bidii humbadilisha mwanadamu taratibu. Huenda leo usione matokeo ya juhudi zako, lakini kila hatua unayopiga ina maana kubwa kwa maisha yako ya kesho.

Wakulima hawavuni siku wanayopanda, wanavumilia jua, mvua, na wakati mwingine ukame, lakini mwisho wake mavuno huja, vivyo hivyo katika maisha ya mwanadamu, kila anayevumilia kwa bidii, ipo siku ataona matunda ya mapambano yake.

 

Tatizo kubwa la kizazi hiki ni kutaka mafanikio ya haraka bila kuvumilia mchakato,watu wengi wanataka kuonekana wamefanikiwa kabla hata hawajajifunza kupambana, wanataka matokeo makubwa ndani ya muda mfupi.

Lakini ukweli wa maisha ni kwamba vitu vikubwa hujengwa kwa muda, mlima haupandwi kwa kuruka, unapandwa hatua kwa hatua na kila hatua inahitaji bidii.

 

Kuna watu leo wanahitaji kusikia maneno haya; kwamba bado hawajachelewa, umri wako si kikwazo cha mafanikio yako, kile ulichopoteza si mwisho wa maisha yako, hata kama dunia imekukatisha tamaa, bado unaweza kuanza upya.

 

Wapo walioanza maisha upya wakiwa hawana chochote, lakini leo wanawahamasisha wengine wasikate tamaa. Kilichowafikisha hapo si miujiza pekee, bali ni maamuzi ya kuendelea kujituma hata wakati mambo yalikuwa magumu.

 

Bidii pia hujenga heshima ya kweli, Dunia humheshimu mtu anayepambana kwa uhalali, Mtu anayechoka kutafuta maisha kwa njia ya haki huwa na amani moyoni kuliko anayekimbilia njia za mkato.

Jasho la bidii lina heshima kubwa kuliko utajiri wa haraka usio na msingi, ndiyo maana watu wengi waliofanikiwa kwa juhudi zao hubaki kuwa mfano wa kuigwa hata baada ya miaka mingi kupita.

 

Katika maisha haya, si lazima uwe mkamilifu ili uanze tena. Unachohitaji ni uamuzi, amua leo kutoruhusu majeraha ya jana yaharibu kesho yako, amua kuinuka tena hata kama uliwahi kuanguka mara nyingi.

Amua kufanya kazi kwa bidii hata kama hakuna anayekupongeza sasa, maana ipo siku dunia itashangaa ulifikaje hapo, bila kujua ni mara ngapi ulianguka na kunyanyuka kimya kimya.

 

Kumbuka, mafanikio hayaendi kwa wenye bahati pekee, bali huenda kwa wale wanaokataa kusimama njiani, maisha yatajaribu kukuzuia, lakini bidii itakufundisha kusonga mbele.

 

Na wakati mwingine ushindi mkubwa wa mwanadamu si kutokuwahi kuanguka, bali ni uwezo wa kusimama tena kila anapoanguka.

 

Hivyo basi, kama leo moyo wako umechoka, kama umekata tamaa, au kama unaona ndoto zako zimefifia, usikubali kubaki chini. Simama tena, Anza tena, Pambana tena.

 

Dunia bado haijaona uwezo wote uliobeba ndani yako. Na huenda kesho yako ikawa ushuhuda mkubwa wa kwamba kweli, bidii inaweza kumbadilisha mwanadamu na kuyageuza maisha yake kabisa.

 
 
 

Comments


bottom of page